Monday, June 4, 2012
JINI LA SARENDA EPISODE 1.
Majira ya saa nane za usiku msichana Suzana alikuwa
akitoka kujirusha katika ukumbi wa Bilicanas.
Kilichomshtua kilikuwa kutoweka kwa mpenzi wake
Sammy ambaye aliondoka bila kumuaga. Wazo lake
la kwanza lilikuwa Sammy kaondoka na msichana
mwingine akijua kabisa yeye ndiye mchumba wake. Akiwa amekasirika kwa kitendo cha Sammy
kuondoka na kumuacha peke yake, kila alipopiga
simu yake iliita bila kupokelewa kitu kilichoonesha
dharau. Aliamua kurudi nyumbani kwake japo
alipanga siku ile kwenda kulala kwa Sammy.
Aliendesha gari akiwa amefura kwa hasira huku machozi yakimtoka kutokana kitendo
alichotendewa na mpenzi wake ambaye ndiye
aliyemtoa kitandani alipokuwa amekwisha kulala.
Suzana awaliza mengi juu ya kitendo cha mpenzi
wake kumwita klabu na kumkimbia. Wakati akitoka Bilicanas mvua ilianza kunyesha,
hakutaka kuisubiri aliamua kwenda nayo ili awahi
kunyumba angalau alale kwa muda mchache ili
asubuhi awahi kanisani misa ya kwanza. Mvua ilikuwa kubwa iliyoambatana na upepo mkali
kitu kilichomfanya ashindwe kuona mbele ilimbidi
alisimamishe gari pembeni ya daraja ya Salenda ili
kusubiri upepo upungue ndipo aendelee na safari
yake. Upepo ule haukuchukua ulitulia na mvua
ilikuwa imekatika. Alipowasha gari liligoma kuwaka, alirudia zaidi ya
mara tano kuzungusha funguo lakini liligoma
kuwaka. Kuteremka kwenye gari alishindwa
kutokana na hali ya kiza cha kutisha nje. Wasi wasi
ulimtawala na kujiuliza atatokaje pale au ndio atalala
mpaka asubuhi. Hasira zilizidi kumpanda Suzana kutokana na
kukimbiwa na mpenzi wake na kuharibikiwa na gari.
Kutokana na hofu aliyokuwa nayo alihakikisha
milango na vioo vyote vimefungwa vizuri. Alijikuta
akipiga dua kumuomba Mungu amuokoe la janga lile
kwa kupata msaada wa watu wenye gari kumsaidia kuwasha gari lake. Lakini kwa muda ule hakukuwa
na dalili ya gari lolote kupita. Akiwa ameinama mikono ameikutanisha kifuani
kwake alishtushwa na upepo makali uliovuka toka
baharini na kulifanya gari lake kuyumba na kusogea
kidogo. Kwa woga uliompata Suzana alijikuta
akitokwa na haja ndogo bila kuelewa. Alitamani
kulia lakini aliamini sauti yake haitasaidia lolote kwa vile hakukuwa na wakumsaidia. Aliinama kwa woga hakutaka kuangalia popote
zaidi ya kusubiri chochote kitakachomtokea. Baada
ya muda hali ile ilitulia, Suzana alinyanyua kichwa
taratibu ili achukue simu ampigie baba yake amfuate
eneo lile ambalo lilikuwa limemuweka katika hali ya
hatari. Aliponyanyua uso achukue simu iliyokuwa kwenye
kwenye dash board, alishtushwa na mwanga mkali
kama jua la saa saba mchana. Aliangalia katikati ya
bahari palipokuwa kunatoka mwanga ule. Alituliza
macho baada ya kumuona mwanamke aliyekuwa
amevaa gauni jeupe lilikuwa liking’aa kutokana na mapambo yake. Hali ile ilimfanya asahau yalitomtokea muda mfupi na
kutuliza macho kumuangalia yule mwanamke
aliyekuwa akitembea juu ya maji huku nyuma
akisindikizwa na wasichana walikuwa wamebeba
vikapu vidogo vilivyokuwa na maua ambayo
walimwagia kila hatua ilivyopigwa huku wakiimba nyimbo nzuri. Suzana alijikuta akipata ujasiri wa ajabu kwa
kufungua dirisha kidogo ili aweze kusikia watu wale
walikuwa wakiimba kitu gani. Zilikuwa sauti nzuri
kama za kaswida zilizoibwa kwa lugha ya kiarabu.
Nyimbo zile zilimvutia na kujikuta akiwa na hamu ya
kuwaona watu wale waliokuwa wakitembea juu ya maji huku kwa mstari mbele akitangulia yule
mwanamke ambaye usoni kwake kulikuwa
kunawaka kama taa na kushindwa kuiona sura
yake vizuri. Suzana alijikuta akisahau kama wale watu walikuwa
wakitembea juu ya maji zaidi ya kushangazwa na
sherehe ile ambayo toka azaliwe hajawahi kuona
sherehe ya aina ile ya mtu mmoja kutangulia mbele
wengine kumfuata nyuma huku wakimuwagia maua
na kumwimbia nyimbo nzuri. Baada ya muda watu wote walikaa mstari mmoja,
kisha yule mwanamke aliyekuwa amepeneza kuliko
wote alipita katikati yao na kupigiwa vilegele huku
akitupiwa maua. Manukato ya maua yalisambaa
mpaka ndani ya gari la Suzana alilokuwa amefungua
kioo kidogo kusikia nyimbo alizokuwa anaimbiwa yule mwanamke ambaye alionekana kama bibi
harusi lakini muda wote hakumuona bwana harusi
wala mwanaume kwenye kundi lile. Yule mwanamke alipita kwenye mstari mpaka
mwisho alitembea peke yake bila kufuatwa na mtu
kisha aligeuka na kuwapungia mkono wenzake
ambao nao walimpungia huku wakimrushia maua.
Baada ya kutembea kidogo Suzana alimshuhudia
yule mwanamke alikunja gauni lake usawa na kifua na kushangaa kumuona akitembea ndani ya maji
yaliyokuwa yamemfika tumboni. Suzana alijikuta akishtuka na kujiuliza yupo ndotoni
au anaona kweli, kilichomshangaza ni umbali
aliotoka yule mwanamke akitembea juu ya maji.
Lakini cha kushangaza alipokaribia ufukweni
alionekana yupo ndani ya maji yaliyomfikia tumboni. Aliendelea kumtazama amuone anakwenda wapi,
yule mwanamke baada ya kutoka ndani ya maji
alitembea juu ya mchanga kulifuata lile gari. Kila
hatua ilivyokuwa akipiga ilizidi kumtisha Suzana,
alijikuta akimshangaa kutaka kuijua sura yake.
Alituliza macho yake kwenye uso wa yule mwanamke aliyekuwa akiisogelea gari huku
manukato makali yakizidi kujaa ndani ya gari. Kilichomshangaza zaidi ni sura ya yule mwanamke
alikuwa akifanana naye kwa kila kitu umbile na sura.
Suzana alishtuka na kufunga kioo haraka ili mtu yule
ambaye yeye alimuona wa muujiza asiingie kwenye
gari. Yule mwanamke alisogea kwenye gari na
kuligusa, ajabu baada ya kuligusa lile gari alitoweka ghafla. Suzana akiwa anatetemeka alijaribu kuwasha gari
kwa mara nyingine, ajabu ya Mungu gari liliwaka
aliondoka eneo lile kwa mwendo wa kasi. Alipofika
nyumbani kulikuwa kumekucha, alikwenda kuoga
haraka ili awahi kanisani kwani muda ulikuwa
umekwenda. Baada ya kuoga alirudi ndani, lakini alishtushwa na
harufu ya manukato ambayo aliyasikia muda mfupi
darajani gari lake lilipozima na kuenea hadi ndani ya
gari lake. Hakutaka kulifikiria sana lile kwa muda
ulikuwa umekwenda, alikwenda kwenye kabati
kubadili nguo ili awahi kanisani. Baada ya kumaliza kubadili nguo alijikuta akiingiwa
na uvivu na kwenda kukaa kwenye kitanda
haikupita muda. Usingizi mzito ulimshika na kulala
bila kujielewa, aliposhtuka usingizini alishtuka
kuiona familia yake yote imesimama mbele yake.
Alijiuliza kuna nini, alipojiangalia alijiona alikuwa amevaa nguo za kuendea kanisani. “Suzana upo sawa?” Mama yake alimuuliza.
“Mbona unaniuliza hivyo? Halafu mbona kama wote
mlikuwa mnalia kuna nini mbona mnanitisha? Nini kimemtokea Suzana mpaka familia yake
ikusanyike mbele yake huku wakitokwa na machozi.
Kuyajua yote fuatana nami katika simulizi hii mpya ya
kusisimua